Mhe. Hussein Bashe Aiwakilisha Tanzania Katika Mkutano wa IFAD

Roma, Italia, Tanzania imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kuimarisha sekta ya kilimo kupitia ushirikiano wa kimataifa, ambapo Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe, alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa 48 wa Baraza la Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD). Mkutano huu wenye kaulimbiu ‘Catalyzing Investment at the First Mile umeangazia umuhimu wa uwekezaji wa awali katika mnyororo wa thamani wa kilimo, hususan kwa wakulima wadogo.

Katika hotuba yake kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Bashe alisisitiza kuwa mkutano huu umekuja wakati muafaka, dunia ikiwa inahitaji mjadala wa wazi kuhusu miundombinu ya kifedha ya kimataifa. Alieleza kuwa Tanzania ina ushirikiano wa muda mrefu na IFAD na itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza sekta ya kilimo inayochangia 70% ya ajira nchini.

Dhamira ya Tanzania Katika Kilimo Waziri Bashe alieleza kuwa Tanzania imechukua hatua kadhaa za kimkakati kuimarisha kilimo, zikiwemo:

  • Kuongeza bajeti ya sekta ya mazao kutoka Dola za Kimarekani milioni 88 mwaka 2021 hadi Dola milioni 420 mwaka 2024.
  • Bajeti ya sekta ya mifugo imeongezeka kutoka Dola milioni 16 hadi Dola milioni 120.
  • Ukuaji wa sekta ya kilimo umeongezeka kutoka 2.7% hadi 4.2% mwaka 2024.
  • Uzalishaji wa chakula umeongezeka kutoka tani milioni 17 hadi tani milioni 22.
  • Thamani ya mauzo ya mazao nje ya nchi imeongezeka kutoka Dola bilioni 1.2 hadi Dola bilioni 3.5.
  • Uhimilivu wa chakula umeongezeka kutoka 114% hadi 128%.

Mikakati ya Maendeleo ya Kilimo 

Tanzania inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya umwagiliaji, ambapo eneo linalomwagiliwa limeongezeka kutoka hekta 560,000 hadi milioni 1.2. Aidha, serikali inalenga kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno kutoka 25% hadi 5% ifikapo mwaka 2030.

Waziri Bashe pia alitangaza kwamba Tanzania inajiandaa kuzindua Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ambayo imeipa sekta ya kilimo nafasi ya kipekee katika mageuzi ya uchumi wa taifa. Katika kufanikisha hili, serikali imeandaa Mpango Mkuu wa Kilimo wa 2050 ambao unatoa mwelekeo wa uwekezaji na hatua mahususi za kuleta mageuzi ya kilimo kwa miaka 25 ijayo.

Ushirikiano wa Kimataifa na IFAD 

Tanzania inatambua mchango mkubwa wa IFAD katika kusaidia miradi ya kilimo nchini, ikiwa ni pamoja na:

  • Programu ya Maendeleo ya Kilimo na Uvuvi.
  • Mradi wa Kilimo Endelevu cha Mifugo.
  • Mradi wa Uhimilivu wa Mfumo wa Chakula wa Tanzania.

Waziri Bashe alitoa shukrani kwa IFAD na wadau wengine wa maendeleo kwa kuendelea kusaidia juhudi za Tanzania katika kilimo. Alisisitiza kuwa ili kuhakikisha kilimo endelevu na ustawi wa uchumi, dunia inapaswa kuwekeza kwa wakulima wadogo kwa kutengeneza mazingira rafiki ya kifedha na kiteknolojia.

Katika hitimisho la hotuba yake, Waziri Bashe alihimiza ushirikiano wa kimataifa katika kurekebisha mifumo ya kifedha duniani ili kuhakikisha kwamba wakulima wadogo wanapata rasilimali na fursa sawa za maendeleo. Alihitimisha kwa kushukuru Rais wa IFAD na wajumbe wa mkutano kwa kuendelea kuunga mkono maendeleo ya sekta ya kilimo nchini Tanzania.

Tanzania imesisitiza nafasi yake kama mshirika muhimu katika juhudi za kimataifa za kuhakikisha usalama wa chakula, ukuaji wa uchumi, na ustawi wa wakulima wadogo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *