🗓️ 17 Desemba 2024
Leo, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb), amekutana na wadau wa tasnia ya mbegu kwa ajili ya kujadili changamoto zinazokabili sekta hiyo na kuimarisha mfumo rasmi wa usambazaji wa pembejeo za kilimo nchini.

Katika kikao hicho, Mhe. Waziri amewataka wazalishaji na wasambazaji wa mbegu kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhamasisha wakulima kujisajili katika mfumo wa usajili wa ruzuku. Mfumo huu wa kidigitali, unaosimamiwa na Serikali, unahakikisha mauziano ya pembejeo yanafanyika kwa njia rasmi, huku ukirahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi na takwimu za usambazaji wa pembejeo kote nchini.
“Mfumo huu tayari unatekelezwa kwa mafanikio katika tasnia ya mbolea, ambapo tumeshuhudia ongezeko kubwa la matumizi kutoka tani 360,000 hadi tani 1,000,000. Kwa sasa, tunaendelea na usajili wa wakulima ili kuwezesha ununuzi wa mbegu za mahindi za ruzuku kwa msimu huu. Mfumo huu utaendelea kutumika katika mauziano ya mbegu za mazao mengine na viuatilifu,“ alisema Mhe. Waziri.
Aidha, Mhe. Waziri amewataka wazalishaji wa mbegu nchini kuwasilisha gharama zao za uzalishaji kwa TOSCI (Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania) ndani ya kipindi cha wiki moja. Hatua hii inalenga kuwezesha utayarishaji wa bei elekezi ya mbegu kuanzia ngazi ya Taifa hadi kijiji.

“Mfumo wa bei elekezi utahakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa bei stahiki, huku tukidhibiti changamoto ya upandishwaji holela wa bei unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu,” aliongeza Mhe. Waziri.
Wizara ya Kilimo itaendelea kushirikiana na wadau wote wa sekta ya kilimo kuhakikisha wakulima wanapata huduma bora, pembejeo za kisasa, na mazingira rafiki ya kuboresha uzalishaji wa mazao nchini.
Kazi Iendelee.