Dodoma, 10 Desemba 2024
Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb), leo amekutana na ujumbe maalum wa wawakilishi kutoka kampuni mbili mashuhuri za Japan—Nasa Corporation, inayojihusisha na utengenezaji wa mashine za kufungasha chai, na Kawasaki Kiko, inayobobea katika utengenezaji wa mashine za kuchakata chai.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini Dodoma yalilenga kubuni njia za kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni hizo ili kuboresha thamani ya zao la chai na kuinua kipato cha wakulima wadogo. Mhe. Waziri amesisitiza kuwa moja ya vipaumbele vya Serikali ni kuhakikisha wakulima wa chai nchini wanapiga hatua kutoka kuuza majani ghafi ya chai mara baada ya kuvuna hadi kuuza chai iliyosindikwa, hatua itakayowapa fursa pana zaidi katika masoko ya kimataifa.
“Nimewahakikishia wawakilishi wa kampuni hizi kuwa Serikali ya Tanzania iko tayari kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Japan pamoja na wadau wa sekta ya chai ili kuhakikisha chai yetu yenye ubora inapata nafasi ya ushindani katika soko la kimataifa, hususan nchini Japan,” amesema Mhe. Waziri.
Kwa kuimarisha ushirikiano huu, ujumbe huo umetangaza mpango wa kutembelea mashamba ya chai katika mikoa ya Iringa, Njombe, na maeneo mengine nchini ili kujionea hali halisi ya uzalishaji wa chai na kuchunguza fursa za kuimarisha zaidi tasnia hiyo.

Ujumbe huu ulio wakilisha kampuni hizo umeongozwa na Bw. Daniel Nganga, Msimamizi wa Mauzo Kanda ya Afrika wa Nasa Corporation; Bi. Gaelle Lagrouas kutoka Idara ya Uzalishaji (Vifungashio na Mauzo Kanda ya Afrika); na Bw. Motohiro Handa, Meneja wa Kitengo cha Usimamizi wa Kawasaki Kiko.
Mhe. Waziri ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wa kimataifa katika jitihada za kukuza kilimo nchini na kuhakikisha wakulima wanapata manufaa makubwa zaidi kupitia uwekezaji wa kiteknolojia katika usindikaji wa mazao.
