Waziri wa Kilimo, Mhe, Hussein Bashe, ametangaza marufuku ya kuingiza nchini mazao ya kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini, baada ya nchi hizo kushindwa kufungua masoko yao kwa bidhaa za kilimo kutoka Tanzania.
Amesema hatua hiyo inalenga kulinda maslahi ya wafanyabiashara wa Tanzania, ambao wamekuwa wakikumbwa na changamoto za kusafirisha mazao yao nje ya nchi, huku nchi hizo zikiendelea kunufaika na soko la Tanzania.

“Kuanzia usiku wa Aprili 23, 2025, zao lolote linalotoka Afrika Kusini au Malawi halitaruhusiwa kuingia nchini. Hii ni hatua ya kulinda biashara yetu na kuonyesha msimamo wa kutaka usawa wa kibiashara kati ya mataifa,” ameeleza Mhe Waziri Bashe
Amefafanua kuwa Malawi imekuwa ikizuia bidhaa kama unga, mchele, tangawizi, ndizi na mahindi kutoka Tanzania, lakini wakati huo huo inanunua mahindi kupitia Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa ajili ya kukabiliana na baa la njaa nchini humo.
“Mahindi yote waliyonunua kupitia WFP kwa ajili ya Malawi hayatapelekwa hadi pale watakapofungua soko lao kwa mazao kutoka Tanzania,” ameonya Mhe Waziri Bashe.
Pia amesisitiza kuwa kuanzia Mei 1, 2025, mbolea iliyopangwa kusafirishwa kwenda Malawi kwa ajili ya msimu wa kilimo haitaruhusiwa kutoka nchini.

“Hatua hii haihatarishi usalama wa nchi wala wa chakula. Hakuna Mtanzania atakayekufa kwa kukosa zabibu au tufaa kutoka Afrika Kusini. Tunachukua hatua hii kwa ajili ya kulinda uchumi na heshima ya nchi yetu,” amesisitiza.
Itakumbukwa kuwa, Aprili 17, 2025, Mhe, Waziri Hussein Bashe alitoa siku saba kwa nchi hizo kuondoa vikwazo vyao dhidi ya bidhaa za Tanzania, akibainisha kuwa endapo hawatafanya hivyo, Serikali ya Tanzania itachukua hatua kali jambo ambalo sasa limetekelezwa rasmi.