Dodoma, 22 Agosti 2025 – Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Mohamed Bashe (Mb), amezindua rasmi Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma, huku akitoa maagizo mahsusi ya kuimarisha usimamizi na ukuzaji wa tasnia ya mbegu nchini.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Bashe ameipongeza Bodi mpya kwa kupewa dhamana ya kusimamia sekta nyeti ya mbegu na kusisitiza wajibu wao wa kuhakikisha Tanzania inapunguza utegemezi wa mbegu kutoka nje ya nchi kwa kuhamasisha na kuendeleza kampuni za ndani zinazozalisha mbegu.
Tunataka kufikia uzalishaji wa tani laki sita za mbegu bora ifikapo mwaka 2030. Hii ni kazi inayowezekana endapo wadau wote wataweka nguvu ya pamoja katika kuzalisha, kusimamia na kuhakikisha mbegu bora zinawafikia wakulima kwa wakati na kwa bei nafuu,” alisema Waziri Bashe.
Kudhibiti tatizo la mbegu feki
Waziri Bashe ametoa maagizo kwa TOSCI kushirikiana kwa karibu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kudhibiti kwa nguvu zote changamoto ya mbegu feki ambayo imekuwa ikiwakwamisha wakulima wengi nchini.

Amesema ni lazima taasisi hizo ziimarishe ushirikiano wa pamoja, kuwatambua na kuwachukulia hatua kali za kisheria wote wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.
“Tatizo la mbegu feki ni janga kwa wakulima wetu. Hatuwezi kuliacha liendelee. Tunataka TOSCI, TAKUKURU na vyombo vingine vya dola washirikiane kuhakikisha kila mkulima anapata mbegu bora na sahihi,” alisisitiza Waziri.

Waziri Bashe pia, ameielekeza TOSCI kufanya kazi kwa karibu na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) ili kuhakikisha kunakuwepo na mikakati ya pamoja yenye malengo ya kuongeza tija na uzalishaji wa mbegu bora nchini.
Mhe waziri amesisitiza kuwa taasisi hizi zinapaswa kuzungumza lugha moja kwa kuweka mipango shirikishi ambayo italeta mapinduzi makubwa katika sekta ya mbegu na kilimo kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Bodi ya TOSCI, Dkt. Lilian Shechambo, alimshukuru Waziri Bashe kwa imani aliyoonesha kwa uteuzi huo na kuahidi kuwa Bodi itatekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi.
“Tumejipanga kushirikiana na Menejimenti ya Wizara ya Kilimo pamoja na wadau wote ili kufanikisha lengo la kuzalisha tani laki sita za mbegu bora ifikapo mwaka 2030. Pia tutaendelea kuimarisha ofisi za kanda za TOSCI ili kuongeza kasi ya utendaji na usimamizi wa mbegu nchini,” alisema Dkt. Shechambo.
Uzinduzi wa Bodi mpya ya TOSCI ni hatua muhimu katika kuimarisha tasnia ya mbegu nchini, kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora, kudhibiti mbegu feki na kuweka mfumo madhubuti wa usajili na usambazaji wa mbegu.
Waziri Bashe ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kuwa sekta ya mbegu inakuwa nguzo ya maendeleo ya kilimo na uchumi wa taifa, sambamba na malengo ya kufanikisha Mapinduzi ya Kilimo Tanzania.
