Tarehe 28 Juni 2025

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Viongozi wa Serikali mliopo,
Mabibi na Mabwana,

Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa leo katika tukio hili muhimu la uzinduzi wa Kiwanda cha Mbolea ITRACOM hapa Dodoma.

Mheshimiwa Rais, takribani miaka minne iliyopita, ulitoa maelekezo mahsusi kuhusu suala la uwekezaji katika uzalishaji wa mbolea nchini. Kufuatia maelekezo hayo, Waziri wa Uwekezaji wa wakati huo, pamoja na Mzee Chiligati na timu yao, walifika ofisi ya Wizara ya Kilimo hata siku ya Jumapili, na hapo ndipo safari hii ya kiwanda hiki ilipoanzia rasmi.

Kwa dhati kabisa, napenda kumshukuru mwekezaji wetu, Mwekezaji ambaye ni mtu jasiri na mwenye uthubutu mkubwa. Tulipomueleza tu kuhusu mahitaji ya kiwanda, hakusubiri ‘feasibility study’. Alituuliza kama Serikali itamuunga mkono, nasi tukasema ndiyo. Aliamini, akachukua hatua. Leo hii tunashuhudia matokeo ya uamuzi wake huo. Kwa niaba ya Serikali, namshukuru pia Majid Nsekela kupitia Benki ya CRDB kwa kushiriki katika kufanikisha uwekezaji huu.

Mheshimiwa Rais, naomba pia nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Anthony Mtaka kwa usaidizi na usimamizi wake tangu akiwa Naibu Waziri. Tulikuja hapa jioni, si kwa ziara rasmi, bali kujadili na menejimenti changamoto walizokuwa wakikumbana nazo. Kesho yake tulikuwa kazini kuzitatua.

Vilevile, naomba kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa sasa wa Dodoma, Dada yangu Rosemary Senyamule. Barabara ya kufika kiwandani ilikuwa haipitiki kabisa. Wizara ya Kilimo haina TANROADS, haina TARURA. Tulimwomba msaada, akaitikia haraka na akasimamia utekelezaji. Leo barabara inapitika na uzalishaji umeanza rasmi.

Nimshukuru pia Mbunge wa Dodoma Mjini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, ambaye tangu akiwa Naibu Waziri alihakikisha mradi huu unasonga mbele. Pia, napenda kumshukuru kwa dhati Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dotto Biteko, kwa maamuzi magumu na ya kizalendo aliyoyafanya wakati akiwa Waziri wa Madini. Alihakikisha leseni ya fosfeti inayohitajika kwa ajili ya kiwanda hiki inapatikana, licha ya changamoto kubwa zilizokuwepo kutokana na uwekezaji wa awali.

Mheshimiwa Rais, naomba pia nikushukuru wewe binafsi kwa kuendelea kutoa uongozi thabiti katika sekta ya kilimo. Jana umehutubia taifa napenda kueleza wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ndiyo imetekeleza kwa vitendo dhana ya kupeleka maendeleo vijijini jambo ambalo tangu enzi za Mwalimu Nyerere lilikuwa kwenye maandiko tu bila utekelezaji.

Nimekuta ofisini maandiko ya wazee wetu, akiwemo Mzee Wasira, aliyekuwa akiandika kwa mapana juu ya umuhimu wa ruzuku, lakini utekelezaji haukuwahi kufanyika. Leo hii tunaona matunda ya kazi zako.

Mheshimiwa Rais, Serikali yako imepeleka maji vijijini, imetoa fedha kupitia TARURA kwa ajili ya barabara za vijijini, na kuhakikisha wakulima wanafikisha mazao yao sokoni kwa urahisi. Leo vijiji vyote zaidi ya 12,000 vina umeme jambo ambalo sisi tuliokulia vijijini tunajua thamani yake.

Serikali yako pia imetoa ruzuku ya zaidi ya Shilingi bilioni 700 kwa mwaka kwa wakulima wa mbolea. Mwaka 2020, matumizi ya mbolea yalikuwa tani 360,000. Msimu wa kilimo uliopita, matumizi yamefikia tani 860,000. Aidha, zaidi ya Shilingi bilioni 500 zimetolewa kwa wakulima wa korosho, ikiwemo ruzuku ya Shilingi bilioni 300 kwa zao hilo. Serikali pia imetoa ruzuku ya tumbaku, na sasa Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa uzalishaji wa tumbaku.

Tuna rekodi ya kihistoria ya kuzalisha zaidi ya tani milioni 12 za mahindi kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tangu tupate uhuru.

Mheshimiwa Rais, mwezi Agosti mwaka jana ulizindua Programu ya Uendelezaji wa Kilimo cha Kisasa (Mechanization Program) ambayo inalenga kuondoa dhana ya mkulima wa heka mbili kununua trekta ya Shilingi milioni 70. Kupitia program hiyo, Serikali inapeleka matrekta 10,000, power tillers 10,000, na vituo vya mechanization 1,000, huku wakulima wakilipiwa gharama kwa mfumo wa ruzuku.

Mheshimiwa Rais, kama ulivyotuambia jana haya ndiyo maendeleo ya vijijini. Na sisi wakulima tuna ajenda yetu mwezi Oktoba: ajenda ya kulinda kiongozi anayelinda maslahi ya wakulima.

Kwa kuhitimisha, Mheshimiwa Rais, nataka niwataarifu Watanzania kuwa tuna mwekezaji mwingine mpya aliyepo mkoani Tabora. Tayari ekari 2,700 zimeanza kuandaliwa kwa ajili ya kulipa fidia ili kujenga kiwanda kipya cha mbolea kitakachotumia malighafi ya makaa ya mawe. Feasibility study imefanywa na Serikali yako. Kiwanda hiki kitazalisha mbolea maalum ya tumbaku, aina ya organo-chemical (organic-mineral).

Baada ya mwaka 2030, nchi yetu haitahitaji tena kuagiza urea kutoka nje. Tutazalisha wenyewe, huku maandalizi ya miundombinu ya gesi yakiendelea. Tanzania itakuwa taifa linalojitosheleza kwa mbolea.

Mheshimiwa Rais, kwa mara nyingine nakushukuru kwa dhamira yako ya kweli ya kuwakomboa wakulima wa Tanzania.