Dodoma: Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, (Mb) amesema kuwa Serikali kupitia Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) inaanza rasmi mchakato wa kusajili mbegu za asili ili ziweze kuingizwa sokoni na kuwapa wakulima uhuru wa kuchagua kati ya mbegu hizo na zile za kisasa.
Mhe. Bashe aliyasema hayo tarehe 15 Mei 2025, wakati wa Mkutano wa Taifa wa Wadau wa Tasnia ya Mbegu uliofanyika jijini Dodoma. Aliposisitiza kuwa baada ya kusajiliwa, mbegu za asili zilizofanyiwa utafiti zitapaswa kupelekwa sokoni haraka, ili wakulima waweze kufanya maamuzi sahihi ya kilimo kulingana na mazingira yao na aina ya uzalishaji wanaolenga.

Waziri Bashe pia aliitaka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa kushirikiana na TOSCI, kuhakikisha mbegu za asili zinapewa kipaumbele sawa na zile za kisasa katika mchakato wa tafiti na usambazaji.
Kwa mujibu wa takwimu, uzalishaji wa ndani wa mbegu nchini unaendelea kuimarika katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo:
- Mwaka 2020/2021 uzalishaji wa ndani ulikuwa tani 34,000 huku tani 15,000 zikiagizwa kutoka nje.
- Kwa msimu wa mwaka 2023/2024, uzalishaji wa ndani umeongezeka hadi tani 56,000 huku uagizaji kutoka nje ukibaki chini ya tani 15,000.
Takwimu hizi zinaonesha mafanikio ya wazi ya ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa kilimo katika kuongeza uzalishaji wa mbegu bora nchini.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kampuni ya AGRA, Bw. Ipyana Mwakasaka, alieleza kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika maeneo ya utafiti, uwekezaji, uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora kwa wakulima.
Naye Bi. Zainabu Masaki, mkulima kutoka Morogoro, aliomba watafiti waboreshe zaidi mbegu za asili ili ziweze kupatikana kwa urahisi sokoni. Alisema baadhi ya wakulima wanajikuta wakitumia mbegu za kisasa kwa lazima kutokana na ugumu wa kupata mbegu za asili.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Hussein Mohamed Omar, pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi.