Tanzania imepata heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Tatu wa Nchi Zinazozalisha Kahawa Afrika (G-25 African Coffee Summit) unaotarajiwa kufanyika tarehe 21-22 Februari 2025 jijini Dar es Salaam. Mkutano huu, ambao awali umefanyika nchini Kenya na Uganda, utahudhuriwa na viongozi na wadau mbalimbali wa sekta ya kahawa barani Afrika. Mgeni rasmi atakuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe (Mb), akizungumza na waandishi wa habari tarehe 14 Januari 2025 jijini Dodoma, ameeleza kuwa mkutano huu utakuwa fursa muhimu kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Waziri Bashe amesema kuwa kupitia mkutano huu, Tanzania itakuwa mwenyeji wa uzinduzi wa “Tamko la Dar es Salaam” (Dar es Salaam Declaration) lenye lengo la kukuza thamani ya zao la kahawa barani Afrika.
Mikakati ya Uwekezaji Kwenye Tafiti na Mafunzo ya Kahawa
Katika kuhakikisha sekta ya kahawa inakua na kuwa endelevu, kupitia mkutano huu Tanzania inatarajiwa kunufaika kwa miradi miwili mikubwa:
- Kituo cha Umahiri na Utafiti wa Kahawa Afrika (Center of Excellence and Research Center for Africa) Kituo hiki, Kitajengwa katika Kituo cha Utafiti wa Kahawa Tanzania (TACRI) kilichopo mkoani Kilimanjaro. Kituo hiki kitakuwa kitovu cha uzalishaji wa miche bora na tafiti za kisayansi kuhusu kahawa barani Afrika.
- Kituo Mahiri cha Mafunzo ya Uzalishaji wa Kahawa (Center of Excellency for Coffee) – Kituo hiki, Kitajengwa mkoani Dodoma na kitawezesha mafunzo ya kitaalam kwa wadau wa kahawa kuhusu teknolojia na mbinu bora za uzalishaji wa zao hili muhimu.

Mafanikio ya Sekta ya Kahawa Tanzania
Mhe, Waziri Hussein Bashe amepongeza juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya kahawa nchini. Amebainisha kuwa uzalishaji wa kahawa umeongezeka kutoka tani 34,000 hadi tani 85,000 mwaka uliopita. Aidha, mauzo ya kahawa nje ya nchi yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 140 hadi zaidi ya Dola milioni 230.
Changamoto na Fursa za Sekta ya Kahawa Afrika
Afrika inazalisha asilimia 50 ya kahawa yote duniani, lakini inachangia Dola za Marekani bilioni 2.5 pekee katika soko la kimataifa, ambalo lina thamani ya Dola bilioni 500. Mhe Waziri Hussein Bashe amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kushirikiana na kuongeza thamani ya kahawa kwa kuachana na uuzaji wa kahawa ghafi na badala yake kuuza kahawa iliyochakatwa.

“Katika miaka 10 ijayo, tunataka asilimia 50 ya kahawa inayozalishwa Afrika iongezewe thamani ndani ya bara hili na kufanikisha biashara huru miongoni mwa nchi zetu,” amesema Waziri Bashe.
Mkutano wa Tatu wa G-25 African Coffee Summit utatoa mwelekeo mpya wa kimaendeleo katika sekta ya kahawa barani Afrika. Kwa Tanzania, mkutano huu si tu utaleta heshima ya kuwa mwenyeji bali pia utaimarisha nafasi yake kama kitovu cha uzalishaji na utafiti wa kahawa barani Afrika. Wadau wote wa sekta ya kahawa wanahimizwa kushiriki kikamilifu na kuchangia mafanikio ya mkutano huu muhimu.