Meatu, 17 Juni 2025 – Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inaendelea kuchukua hatua thabiti kuhakikisha kuwa wakulima wa pamba nchini wananufaika moja kwa moja na jasho lao, kwa kuweka mazingira wezeshi ya soko, thamani na bei.

Akiwa pamoja na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein M. Bashe ameungana na wananchi wa Wilaya ya Meatu kushuhudia uzinduzi wa kiwanda cha kisasa cha kuchakata pamba cha BioSustain Tanzania Limited.
Kiwanda hicho, kilichozinduliwa leo na Rais Samia, ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuongeza thamani ya mazao ya kilimo nchini, hasa pamba – zao ambalo limeingizwa rasmi kwenye orodha ya mazao ya kimkakati. Kikiwa na uwezo wa kuchakata tani 500 kwa siku na kuhifadhi hadi tani 12,000 za pamba ghafi, kiwanda hicho kinatumia teknolojia ya kisasa inayochochea tija na ufanisi mkubwa.

Kupitia uwekezaji huo mkubwa, serikali imefanikiwa kuongeza bei ya ununuzi wa pamba kutoka bei elekezi ya shilingi 1,150 hadi shilingi 1,200 kwa kilo, ikiwa ni ongezeko la shilingi 50 kwa kilo hatua inayolenga kuongeza kipato cha mkulima wa kawaida na kukuza uchumi wa vijijini.
Waziri Bashe amesisitiza kuwa, kupitia ushirikiano wa karibu na sekta binafsi, serikali itaendelea kuhakikisha bei ya pamba inaimarika karibu kila msimu, kwa kuzingatia gharama halisi za uzalishaji, hali ya soko na mahitaji ya wakulima.

Kiwanda hicho pia kimetoa ajira 1,205, kati ya hizo 375 ni ajira za kudumu na 830 ni ajira za msimu hatua inayoonesha mchango wa sekta ya kilimo katika kukuza ajira na kuondoa umasikini. Vilevile, kiwanda hicho kimewezesha maafisa ugani 75 kwa kuwapatia pikipiki na mafuta lita 5 kwa wiki ili kuwafikia wakulima kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
“Dira yetu ni kuhakikisha kilimo cha pamba kinabadilisha maisha ya wakulima, si kwa maneno bali kwa hatua kupitia soko la uhakika, bei nzuri, ajira, na teknolojia. Tunapokwenda kuongeza thamani ya mazao yetu ndani ya nchi, tunaongeza mnyororo wa faida kwa kila mdau wa kilimo.”
Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea na azma yake ya kuinua sekta ya kilimo kama nguzo kuu ya maendeleo ya uchumi wa Taifa. Kwa upande wa pamba, serikali tayari imeanza mchakato wa kuhakikisha Tanzania inasafirisha bidhaa zilizoongezwa thamani, badala ya kuuza pamba ghafi, ikiwa ni sehemu ya ajenda ya nchi ya kuwa na uchumi wa viwanda.