Serikali Yatoa Bilioni 13 kwa Ruzuku ya Tumbaku.

Dodoma, 29 Januari 2025 – Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekabidhi hundi ya Shilingi Bilioni 13 kwa Chama cha Ushirika cha Tobacco Cooperative Joint Enterprises Limited (TCJE) ili kugharamia ruzuku ya wakulima wa tumbaku nchini na kupunguza gharama za uzalishaji. Hatua hii ni sehemu ya mageuzi makubwa yanayoendelea katika sekta ya tumbaku, ambayo yamechangia kuimarika kwa kipato cha wakulima na ongezeko la uzalishaji wa zao hili muhimu.

Katika kipindi cha mageuzi haya, pato la mkulima wa tumbaku limeongezeka kutoka wastani wa Dola 1 hadi Dola 2.3 kwa kilo, huku uzalishaji wa tumbaku ukipanda kutoka chini ya tani 50,000 hadi tani 122,000. Matokeo yake, mapato ya wakulima yamefikia Dola Milioni 269, na mauzo ya nje kufikia Dola Milioni 484, kiwango ambacho kwa mara ya kwanza kimevuka Dola Milioni 400. Mafanikio haya yameifanya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa uzalishaji wa tumbaku barani Afrika, ikitanguliwa na Zimbabwe.

Katika upande wa mbolea, mageuzi ya mfumo wa ruzuku yameleta matokeo chanya, ambapo matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 360,000 kabla ya ruzuku hadi tani 840,000 katika msimu uliopita. Lengo la serikali kwa msimu huu ni kufikisha tani 1,000,000. Aidha, matumizi ya mbolea kwa ekari yameongezeka kutoka kilo 15 hadi kilo 24 mwaka jana, na serikali inalenga kufikia kilo 50 ifikapo mwaka 2030 ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima wa tumbaku na sekta ya kilimo kwa ujumla ili kuongeza uzalishaji, tija na kipato cha wakulima, na kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta hii muhimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *