Simiyu, 16 Juni 2025 – Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein M. Bashe, ameweka msisitizo mkubwa katika mageuzi ya kilimo cha pamba nchini, baada ya kushiriki uzinduzi wa viwanda viwili vya kuchakata pamba na kutengeneza mabomba katika eneo la Salunda, Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu.

Uzinduzi huo umefanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni hatua muhimu ya kuongeza thamani ya mazao ya wakulima wa pamba.

Akiwa mkoani humo, Mhe. Bashe alitangaza kuwa zao la pamba sasa limeingia rasmi kwenye orodha ya mazao ya kimkakati ya taifa, sambamba na korosho, kahawa na mbaazi. Alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kuwa mazao yanayolimwa kwa wingi na wakulima wetu yananufaisha wakulima wenyewe, kupitia kuongeza thamani, ajira, na upatikanaji wa masoko ya uhakika.

Viwanda hivyo viwili, vilivyozinduliwa vinamilikiwa na kampuni ya Moli Oil Mills Co. Ltd, huku vikiwa vimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 8 na tayari vimezalisha ajira zaidi ya 1,200, ikiwa ni pamoja na ajira 850 za moja kwa moja. Aidha, wajasiriamali wadogo wamenufaika kupitia shughuli mbalimbali kama vile mama lishe, wauzaji wa vifaa vya kazi na usafirishaji wa bidhaa.

Mhe. Bashe, amebainisha kuwa mageuzi haya yana lengo la kusitisha kabisa usafirishaji wa pamba ghafi nje ya nchi, badala yake kuchakata na kutengeneza bidhaa za mwisho hapa hapa nchini, ili kuongeza kipato cha mkulima na kuimarisha viwanda vya ndani.

Waziri Bashe ameongeza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira bora kwa wakulima na wawekezaji katika mnyororo wa thamani wa pamba, ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo bora, masoko ya uhakika, pamoja na kuimarisha taasisi za ushirika katika maeneo yote yanayozalisha zao hilo.

Kwa ujumla, Waziri Bashe akiwa katika Ziara ya Mhe Rais mkoani Simiyu ameonesha dhamira ya serikali ya kuweka kipaumbele katika kuinua kilimo cha pamba kupitia viwanda, ushirika, na uwekezaji wa kimkakati ikiwa ni sehemu ya maono mapana ya kufikia Tanzania ya viwanda kwa vitendo.