Dodoma, 12 Mei 2025 – Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb), amekabidhi magari 38 yenye thamani ya shilingi bilioni 4.2 pamoja na mitambo 7 ya uchimbaji visima kwa taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Kilimo. Lengo la makabidhiano haya ni kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya kisekta na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wakulima kote nchini.

Katika makabidhiano hayo:
- Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imekabidhiwa magari 14 kwa ajili ya kusimamia na kudhibiti utoroshaji wa mazao katika maeneo ya mipakani.
- Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) limepokea magari 5 kwa ajili ya kufuatilia usimamizi wa vyama vya ushirika na vyama vya msingi.
- Bodi ya Mkonge Tanzania imekabidhiwa magari 2 kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa shughuli za tasnia ya mkonge nchini.
- Wizara ya Kilimo yenyewe imepokea magari 20 yatakayotumika katika shughuli za kiutendaji na ufuatiliaji wa miradi ya kilimo katika maeneo mbalimbali.

Aidha, mitambo 7 ya uchimbaji visima imekabidhiwa kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kwa ajili ya kuchimba visima kwa wakulima, hususan wakulima wadogo. Mitambo hiyo ina uwezo wa kuchimba visima hadi kina cha mita 300, huku mingine ikiwa na uwezo wa kufikia mita 1,800. Lengo ni kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, hivyo kukuza uzalishaji na kupunguza utegemezi wa mvua.
Waziri Bashe amesema kuwa hatua hii ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha sekta ya kilimo kupitia mpango wa Agenda 10/30, ambao unalenga kuongeza tija na kipato kwa mkulima.

Vilevile, ameeleza kuwa sambamba na ruzuku ya mbegu na mbolea, Serikali sasa inaongeza wigo wa ruzuku kwa wakulima kwa kujumuisha huduma za uchimbaji visima pamoja na upatikanaji wa zana za kilimo.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo:
- Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb)
- Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli
- Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Hussein Mohamed Omar
- Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mariam Ditopile (Mb)
- Menejimenti ya Wizara ya Kilimo
- Watendaji kutoka taasisi na bodi mbalimbali za wizara
Makabidhiano haya ni sehemu ya mwendelezo wa jitihada za kuifanya sekta ya kilimo kuwa ya kisasa, ya kibiashara na yenye tija kwa maendeleo ya Taifa.
