Mgombea Ubunge wa Nzega Mjini na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ametaja sababu tano zinazowafanya wananchi wa Tabora kumpigia kura Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa CCM Samora, Nzega, Bashe amesema wananchi wa Tabora hawatampigia kura Rais Samia kwa sababu tu ni mgombea wa CCM, bali kwa kazi kubwa ambazo tayari zimefanyika katika sekta kuu za maendeleo ya taifa.
Sababu kuu tano ambazo ametaja ni uboreshaji wa elimu, afya, maji, umeme na kilimo. Katika elimu, ameeleza kuwa idadi ya sekondari imeongezeka kutoka shule nne wakati wa uchaguzi uliopita hadi shule 16 leo, na hakuna kata isiyo na shule ya sekondari. Aidha, serikali imetoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika shule za vijijini.

Katika sekta ya umeme, Bashe amesema kuwa miaka iliyopita kata mbili pekee ndizo zilikuwa na huduma ya umeme, lakini sasa kata zote kumi na vijiji vyote 21 vina umeme huku vitongoji vilivyobakia vikitarajiwa kumaliziwa na wakandarasi walioko kazini. Ameongeza kuwa mtandao wa barabara nao umeongezeka kutoka kilomita 160 hadi zaidi ya kilomita 517, hatua inayoashiria kasi kubwa ya maendeleo ya miundombinu.
Sekta ya maji nayo imepewa kipaumbele ambapo, sambamba na huduma kwa wananchi, programu mpya za magati ya maji zimeanzishwa kuhakikisha mifugo inapata maji safi kutoka Ziwa Victoria. Katika sekta ya afya, amefafanua kuwa Hospitali ya Wilaya ya Nzega imeboreshwa kwa kujengewa wodi za kinamama na watoto, vifaa vya kuhudumia watoto njiti na jengo jipya la kuzalisha hewa ya oksijeni, hatua iliyosaidia kuondoa changamoto kubwa zilizokuwa zikikabili akinamama na wagonjwa.

Kuhusu kilimo, Bashe ameeleza kuwa ruzuku ya zaidi ya shilingi bilioni 13 imetolewa kwa wakulima wa tumbaku, huku mauzo ya zao hilo yakifikia zaidi ya dola milioni 416 za Marekani na uzalishaji kufikia tani 1,888, kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa tangu uhuru.
Aidha, amesema kwa wananchi wa Nzega tafsiri ya maendeleo ni barabara vijijini, shule vijijini, umeme vijijini, maji vijijini na ruzuku za pembejeo kwa wakulima. Ameweka wazi kuwa wananchi wa jimbo hilo wamepanga kujitokeza kwa wingi kupiga kura, lengo likiwa ni kufikia zaidi ya asilimia 90 ya wapiga kura.

Bashe pia amesisitiza mshikamano na utii wake kwa Rais Samia, akieleza kuwa dhamira ya Rais katika kuinua wakulima ndiyo sababu kubwa inayowafanya wananchi wa Tabora kumuunga mkono kwa dhati.