Dodoma, 10 Aprili 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi Benki ya Ushirika Tanzania (Coop Bank Tanzania) tarehe 28 Aprili 2025, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kufufua benki za kijamii zilizokuwa zimefilisika nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dodoma, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb.), amesema kuwa hatua hii ni utekelezaji wa maelekezo mahsusi ya Mheshimiwa Rais kwa Wizara ya Kilimo kuhakikisha kuwa benki za ushirika zinarejea kwa nguvu mpya na kuanza kutoa huduma kwa wananchi, hususan wakulima.

Benki ya Ushirika Tanzania inatarajiwa kuanza na matawi manne yaliyopo katika mikoa ya Dodoma, Mtwara, Kilimanjaro na Tabora. Waziri Bashe ameongeza kuwa katika awamu ya pili, matawi ya ziada yataanzishwa katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya na Katavi.

Aidha, mafunzo kwa mawakala wa benki yanaendelea kote nchini ili kuhakikisha huduma za benki zinawafikia wananchi hata katika maeneo ambayo hayana matawi ya moja kwa moja.

Katika kuelekea uzinduzi huo, Kongamano la Wanaushirika litafanyika tarehe 27 Aprili 2025, likitanguliwa na shughuli mbalimbali za kuhamasisha ushiriki wa wananchi.

Waziri Bashe amesisitiza kuwa hatua hii inalenga kuwainua wakulima na jamii kwa ujumla kwa kuwapatia benki rafiki zitakazowasaidia kupata huduma za kifedha kwa urahisi zaidi, tofauti na changamoto walizokuwa wakikumbana nazo katika benki za kibiashara.

“Lengo hapa ni kuhakikisha wakulima wetu wanapata benki zinazowahusu moja kwa moja, zenye masharti rafiki na zinazotoa huduma kwa kuzingatia uhalisia wa maisha ya mkulima,” amesema Mhe. Bashe.

Katika hatua nyingine, Waziri Bashe amesema Wizara ya Kilimo kwa sasa inaendelea na majadiliano na Wizara ya Fedha na Mipango kuhusu haja ya kuiwezesha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kutekeleza majukumu yake ya msingi kama benki ya maendeleo badala ya kufanya kazi kama benki ya kibiashara.

“TADB ni benki ya maendeleo ya kilimo, si ya biashara. Mikopo yake inapaswa kuwa na masharti rafiki zaidi kwa wakulima, si ya miaka miwili au mitatu inayowaumiza,” ameongeza.

Mhe. Bashe ametoa wito kwa washiriki wa sekta ya ushirika na wakulima kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kongamano hilo na kutumia fursa ya kuzinduliwa kwa Benki ya Ushirika ili kunufaika na huduma zitakazotolewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *