Rais Dkt. Samia: Afrika ishirikiane kuleta mageuzi ya kilimo cha kahawa.

Tanzania imeandika historia kwa kuwa mwenyeji wa Kilele cha Mkutano wa Tatu wa Nchi Zinazozalisha Kahawa Barani Afrika, uliofanyika tarehe 22 Februari 2025. Akiwahutubia viongozi na wadau wa sekta ya kahawa kutoka mataifa mbalimbali, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa Afrika lazima ishirikiane katika kuleta mageuzi ya kiteknolojia ili kufanya kilimo cha kahawa kuwa cha kisasa, chenye tija, na chenye mvuto kwa kizazi kipya kushiriki kikamilifu katika ustawi wa uchumi wa Bara la Afrika.

Kwa sasa, takribani asilimia 90 ya mapato yatokanayo na mauzo ya kahawa nje ya Afrika yanatokana na kahawa ghafi. Hali hii imeendelea kusababisha upotevu wa fursa za kiuchumi kwa nchi wazalishaji, huku mataifa ya nje yakijipatia faida kubwa kwa kusindika na kuuza bidhaa za kahawa zenye thamani zaidi.

Katika kufanikisha mageuzi ya sekta hii, Rais Samia ameeleza kuwa Afrika inapaswa kuweka mikakati ya kuongeza thamani ya kahawa kabla ya kuiuza nje. Amesema kuwa ifikapo mwaka 2030, lengo ni kuhakikisha nusu ya kahawa inayozalishwa Afrika inauzwa ndani ya Bara hili kwanza, hatua itakayochochea ukuaji wa viwanda vya usindikaji, kuongeza thamani ya bidhaa, na kuwanufaisha wakulima wa Kiafrika moja kwa moja.

Rais Samia pia amebainisha jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuinua tasnia ya kahawa, akieleza kuwa bajeti ya Wizara ya Kilimo imeongezeka kutoka Dola za Marekani Milioni 107.9 mwaka 2021 hadi Dola za Marekani Milioni 473.3 mwaka 2024. Ongezeko hili linalenga kuimarisha sekta ya kilimo kwa kutoa ruzuku, kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora, pembejeo za kisasa, na kuimarisha utafiti wa kilimo ili wakulima wanufaike zaidi na sekta hii muhimu.

Tanzania inasalia kuwa mshirika madhubuti wa mataifa mengine ya Kiafrika katika kufanikisha mapinduzi ya kilimo cha kahawa kwa maendeleo ya Bara zima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *