


Leo, nimehudhuria mkutano muhimu wa wadau wa kilimo Dodoma, katika Ukumbi wa Mabeho, ambapo tumekuja pamoja kujadili Sera ya Maendeleo ya Benki 2024 na Sera ya Taifa ya Bima 2024. Mkutano huu umegusia haja ya kuwa na sera za moja kwa moja zinazohusiana na mitaji, ugharamiaji, na bima katika sekta za uzalishaji kama kilimo, mifugo, na uvuvi.
Nimewasisitiza wadau kuwa, katika kipindi hiki ambacho tunaye Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni msingi wa mageuzi yetu katika sekta hizi, ni muhimu tushirikiane kutafuta sera maalum zitakazofafanua jinsi mkulima au mfugaji anavyoweza kupata mtaji, maelezo ya riba, bima, dhamana, na muda wa mkopo. Hii ni ili kuendana na juhudi kubwa za uwekezaji zinazofanywa na Mheshimiwa Rais katika sekta hizi za uzalishaji.
Ni msimamo wetu kwamba, mchakato wa kuleta Sera ya Maendeleo ya Benki na Sera ya Taifa ya Bima, ambazo zinajadili sekta za uzalishaji kwa ujumla, zinafifisha juhudi zetu za kimapinduzi katika sekta hizi zinazochangia zaidi ya asilimia 26 ya uchumi wetu na kuajiri Watanzania zaidi ya asilimia 65.
Nashukuru kuwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ameliona hili na kusimamisha mchakato huo mpaka pale tutakapokamilisha Dira ya Taifa, ili tuweze kuja na Sera ya kipekee itakayozinufaisha sekta hizi za uzalishaji yaani kilimo, mifugo na uvuvi.