Katika hatua kubwa ya kuimarisha ulinzi wa mazao na kuwalinda wakulima dhidi ya visumbufu shambani, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amepokea rasmi ndege maalum ya kilimo aina ya Thrush 510 P2 katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma. Ndege hiyo yenye thamani ya Shilingi bilioni 6 imeletwa kwa ajili ya kudhibiti wadudu waharibifu wa mimea kama nzige na kwelea-kwelea.

Ndege hiyo ina uwezo wa kubeba lita 1,930 za viuatilifu kwa wakati mmoja na kunyunyizia dawa katika eneo la zaidi ya ekari 2,400 kwa mzunguko mmoja. Pia Ndege hiyo inaweza kukaa angani kwa zaidi ya saa nne mfululizo, huku tangi lake la mafuta likiwa na ujazo wa lita 86, uwezo mkubwa unaoiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kupambana na changamoto za kilimo zinazosababishwa na wadudu waharibifu.
Mhe. Bashe alisema ununuzi wa ndege hii ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali kwa wakulima, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha kilimo kupitia teknolojia za kisasa. Pia, Mhe waziri ameelekeza kuanza mara moja kwa mchakato wa ununuzi wa ndege nyingine tatu kwa ajili ya vituo vya kilimo anga vilivyopo Arusha, Mbeya-Songwe na Mwanza.
“Nchi lazima iwe na uwezo wa kujitegemea. Dunia ya kubebana imepitwa na wakati. Tayari tumeanza ununuzi wa drones za uchunguzi na mwaka huu tunanunua pia drones za kunyunyizia dawa. Haya yote ni kwa ajili ya kumlinda mkulima na kuongeza tija ya kilimo.

Aidha, Mhe. Bashe, amesema kuwa tayari bajeti ya ununuzi huo imetengwa, na tofauti na awali, mchakato mpya utaharakishwa kwa ufanisi zaidi ili kuhakikisha kila kituo kinapata vifaa vyake mapema.
Pamoja na ndege hizo, serikali ipo mbioni pia kuanza kutumia drones za uchunguzi na kunyunyizia viuatilifu, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kiteknolojia wa kudhibiti visumbufu kwa haraka na kwa usahihi mkubwa.
Katika hatua nyingine, serikali inatarajia kuanzisha vituo 36 vya kisasa vya utoaji wa takwimu na taarifa za visumbufu vya mimea na ndege waharibifu, ili kuongeza kasi na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wakulima.
Mhe. Bashe ameongeza kuwa maeneo kama Bahi, Chemba, Kondoa, na Kongwa yamekuwa yakikumbwa mara kwa mara na mashambulizi ya nzige na kwelea-kwelea, hivyo ujio wa ndege hii ni mkombozi mkubwa kwa wakulima wa maeneo hayo.

Ndege hiyo ilirushwa kutoka Jimbo la Georgia, Marekani na rubani Gian, ambaye alitumia saa 50 kufanikisha safari hiyo.
Hatua hii ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza katika mbinu za kisasa za kilimo, kwa lengo la kuwalinda wakulima, kuongeza uzalishaji na kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea kilimo imara na endelevu.