Ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, sekta ya kilimo imepiga hatua kubwa. Takwimu zinaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani 17,148,290 mwaka 2021/2022 hadi tani 22,803,316 mwaka 2023/2024. Pia, jitihada za Tanzania kuwa “regional basket” zimesababisha utoshelevu wa chakula kupanda kutoka 114% mwaka 2022/2023 hadi 128% mwaka 2024/2025.

Sambamba na hilo, uzalishaji wa mazao ya biashara umeongezeka kwa 44%, kutoka tani 898,967 mwaka 2021 hadi tani milioni 1.3 mwaka 2023. Mazao yaliyoonyesha ongezeko kubwa ni kahawa, korosho, pamba, na alizeti. Vilevile, thamani ya mauzo ya mazao nje ya nchi imeongezeka kutoka dola bilioni 1.48 mwaka 2019/2020 hadi dola bilioni 3.54 mwaka 2023/2024, huku mahindi, mchele, na maharage yakiongoza kwa kusafirishwa kwa wingi.

Mradi wa BBT Umefikia Wapi?

Mradi wa Building a Better Tomorrow (BBT) ni mojawapo ya juhudi za makusudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo. Kupitia bajeti ya Wizara ya Kilimo, ambayo imefikia trilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali inaendelea kuwezesha vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika kilimo kama uwekezaji wa muda mrefu.

Vipengele Muhimu vya Mradi wa BBT

Mradi huu una vipengele vitano muhimu vyote vikilenga kuwawezesha vijana na wanawake katika sekta ya kilimo:

  1. Mashamba Makubwa ya Pamoja (BBT Block Farms)
  2. Utoaji wa Mitaji kwa Vijana na Wanawake
  3. Uchimbaji wa Visima kwa Wakulima Wadogo
  4. Huduma za Ugani
  5. Uongezaji Thamani wa Mazao

Hatua Zilizofikiwa Kufikia Januari 2025

  • Jumla ya ekari 340,244.98 zimetengwa kwa ajili ya kilimo cha vijana, ikilinganishwa na ekari 300 zilizokuwepo wakati wa uzinduzi wa programu.
  • Vijana 686 tayari wanazalisha kwenye mashamba ya Chamwino, Dodoma (Chinangali na Ndogowe).
  • Programu inaendelea na uwekezaji katika umwagiliaji, usambazaji wa pembejeo, na utoaji wa mikopo kwa wakulima vijana.

Vijana Waliopata Manufaa Kupitia BBT

Hadi Desemba 2024, jumla ya vijana na wanawake 43,163 wamenufaika moja kwa moja kupitia vipengele vyote vitano vya programu ya BBT, kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, taasisi zake, na wadau wa maendeleo.

Matokeo ya Awamu ya Kwanza

  • Vijana 686 wameanza uzalishaji katika mashamba ya Chamwino, Dodoma.
  • Shamba la Chinangali (ekari 1,772) linazalisha mbegu za alizeti, pilipili, mtama, maharagwe kunde, na mahindi.
  • Vijana 249 wamepatiwa mafunzo ya usambazaji mbolea na uzalishaji wa mbegu bora.
  • Katika shamba la Ndogowe, vijana 418 wamekabidhiwa ekari 10 kila mmoja kwa ajili ya kilimo cha kisasa.
  • Kituo Atamizi cha Mkonge Tanga na Zanzibar kimewezesha vijana 344 kuzalisha bidhaa za mkonge.

Uwekezaji na Thamani ya Mradi

Serikali na wadau wa maendeleo wamewekeza jumla ya TZS 2.64 trilioni kwa kipindi cha 2022-2030. Kati ya fedha hizo, 24% zinatoka serikalini, huku 76% zikichangiwa na sekta binafsi na washirika wa maendeleo.

Katika msimu wa 2024/2025, kipato tarajiwa kutokana na mradi huu ni faida ya TZS 1.94 bilioni baada ya gharama za uendeshaji.

Hatua Zinazofuata

BBT inaendelea kupanua wigo wake kwa:

  • Kuanzisha mashamba mapya kama Mapogoro-Chunya (ekari 51,528.5).
  • Kuendeleza ujenzi wa miundombinu kama mabwawa ya umwagiliaji, barabara, na minara ya mawasiliano.
  • Kuendelea na utoaji wa mikopo kwa vijana, ambapo hadi Desemba 2024 maombi ya mikopo yenye thamani ya TZS 21.3 bilioni yalipokelewa, huku TZS 5.24 bilioni zikiwa katika hatua za kutolewa.
  • Kufikia ngazi ya halmashauri, ambapo ekari 148,563.91 zimetengwa kwa ajili ya programu ya BBT.

Hitimisho

Mradi wa BBT umeleta mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo, hasa kwa vijana na wanawake. Kupitia uwekezaji mkubwa, tija katika kilimo imeongezeka, vijana wamepata ajira, na taifa limepiga hatua katika kufanikisha malengo ya kuwa “regional food basket”. Serikali inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuimarisha soko la mazao na kuhakikisha vijana wengi zaidi wanajumuishwa katika kilimo cha kisasa na endelevu.

Kwa pamoja, tunajenga mustakabali bora kupitia kilimo kama uwekezaji wa muda mrefu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *