Salaam ndugu zangu,

Ninatumia nafasi hii kumshukuru Allah kwa kila jambo na baraka zake katika safari yangu ya utumishi.

Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa aliyonionyesha katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi kama Naibu Waziri, na hatimaye kuniteua kuwa Waziri wa Kilimo. Ni heshima kubwa niliyothamini kwa moyo wangu wote, na ninaendelea kuwa mwenye shukrani kwa nafasi hii ya kuwatumikia Watanzania.

Natoa pongezi za dhati kwa ndugu yangu Daniel Godfrey Chongolo kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo. Nafahamu kabisa utu wake kama mzalendo na mkulima wa kweli, na nina uhakika atamsaidia Mheshimiwa Rais kutimiza matarajio ya Watanzania. Vilevile, nampongeza ndugu yangu David Silinde kwa kuendelea kuaminiwa kama Naibu Waziri. Sina shaka kwamba atakuwa msaada mkubwa kwa Waziri wake na Wizara kwa ujumla.

Nawashukuru pia watumishi wote wa Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano wa hali ya juu mlionipa katika kipindi cha miaka sita iliyopita. Nawatakia heri na fanaka katika kuendelea kutekeleza majukumu yenu ya kuwatumikia wananchi kwa bidii na uadilifu.

Asanteni sana.