Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, amebainisha kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa letu la  Tanzania limefanikiwa kuuza nje ya nchi sukari tani 80,000, hatua inayoashiria mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya kilimo na viwanda.

Akizungumza mjini Bukoba tarehe 16/10/2025 wakati wa mkutano wa kampeni wa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Bashe amesema kuwa awali, taifa letu lilikuwa likizalisha tani 367,000 pekee za sukari, lakini sasa uzalishaji umeongezeka na kufikia zaidi hadi kufikia tani 630,000.

“Wakati Mhe. Dkt. Samia anaingia madarakani, uzalishaji wa sukari ulikuwa mdogo sana, lakini kutokana na sera bora za Serikali yake, leo tunazalisha zaidi ya tani 630,000. Hii imetuwezesha kuuza nje tani 80,000 za sukari, zikileta nchini zaidi ya Dola za Marekani milioni 72 (sawa na takribani Shilingi bilioni 196.6),” amesema Bashe.

Mhe Bahse ameeleza kuwa Kiwanda cha Sukari cha Kagera kimechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio hayo, ambapo uzalishaji wake umefikia zaidi ya tani 150,000, na upanuzi wa kiwanda hicho unaendelea, ukiwa na matarajio ya kuzalisha hadi tani 200,000 ifikapo miaka miwili ijayo.

Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kilimo cha umwagiliaji katika mkoa wa Kagera, ikiwemo hekta 16,000 za kilimo cha umwagiliaji na mabwawa zaidi ya 10 kwa ajili ya kuhifadhi maji. Mradi huo unakadiriwa kugharimu zaidi ya Shilingi bilioni 500, na unalenga kuwanufaisha wakulima wa wilaya za Bukoba Vijijini, Muleba, Misenyi na Karagwe.

Mhe Bashe pia ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitoa ruzuku ya mbolea, miche ya mazao ya biashara pamoja na fedha kwa wakulima wadogo, hatua iliyowezesha sekta ya kilimo kuongezeka tija na kuimarika kwa uzalishaji katika mazao kama miwa, kahawa, mpunga, vanilla, na tumbaku.

“Kuna watu walihoji kwa nini tunauza sukari nje ya nchi, lakini ukweli ni kwamba hii ni biashara. Kama tuna uwezo wa kuzalisha zaidi ya tunavyotumia, ni busara kuuza ziada nje ili kupata fedha za kigeni. Ndiyo maana leo tunapata Dola milioni 72 kutoka kwenye zao hili pekee,” alisema Bashe.

Ameongeza kuwa hatua hii imesaidia kupunguza upungufu wa sukari nchini, kutuliza bei katika soko la ndani, na kuongeza kipato cha wakulima, jambo linalodhihirisha matokeo ya sera bora za Serikali ya Awamu ya Sita.