Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mridoko amefungua Kongamano la Wadau wa Umwagiliaji na mnyororo mzima wa Sekta ya Kilimo tarehe 19 Julai 2024 katika skimu ya umwagiliaji ya Mwamkulu, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Mkoa wa Katavi. 

Ameeleza kuwa kuna miradi takribani 29 katika Mkoa wa Katavi, ikiwemo miradi mikubwa ya umwagiliaji iliyopo katika maeneo ya Usese na Mwamkulu.  Mhe. Mridoko amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha Sekta ya Kilimo hususan kuhusu bei za Mazao ya kimkakati kama vile Tumbaku, Pamba, Mazao ya chakula na biashara ambayo kwa ujumla bei zimeimarika.

Amepongeza maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia ya Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA) ya kununua mahindi kwa wakulima kwa bei ya kilo kwa shilingi 700, huku gunia la kilo 100 likinunuliwa kwa shilingi 70,000 kuanzia tarehe 18 Julai 2024.

Kuhusu umwagiliaji, Mkuu wa Mkoa wa Katavi amesema kuwa uwepo wa Bw. Raymond Mndolwa, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) umedhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha skimu za umwagiliaji zinawafikia wakulima nchi nzima.  Ameeleza kuwa kuna zaidi ya hekta 124,000 zinazofaa kwa shughuli za umwagiliaji katika Mkoa wake. Ameomba Wadau kutumia ipasavyo Kongamano hilo ili kuwa na uelewa wa pamoja kama Mkoa kuhusu taratibu, sheria na kanuni za kilimo cha umwagiliaji. 

“Niwashukuru Wizara ya Kilimo na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kuleta miradi mizuri kwa manufaa mapana ya wananchi wa Mpanda. Hongereni kwa watu wa Mwamkulu na Nguvumali kwa kutoa ardhi kuwezesha skimu ya umwagiliaji,” amesema Mhe. Mridoko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *