Mheshimiwa Rais, mambo mengi umetoa maelekezo kuwa unataka matokeo, hutaki mambo mengine. Siwezi kurudi kwako kukwambia Mheshimiwa Rais nimekwama kwa sababu utaratibu ulikwama. Hili la Ushirika kuwa na benki katika taratibu za kawaida leo tusingekuwa na benki hii. Nawashukuru sana wote ambao wamefanya tumefikia hapa.

Naomba nimshukuru sana Babu, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambaye sasa yupo Ruvuma, kwa kuibadilisha Tandahimba Community Bank kwenda kuwa Cooperative Bank ili benki hizi mbili ziungane. Ulikuwa mtihani, na siasa za korosho unazifahamu. Lakini niwashukuru Wanaushirika. Mheshimiwa Rais, ulivyoagiza ukasema asilimia 51 ishikiliwe na Ushirika, hatukuwa na shilingi wakati huo. Tulijifungia vyama vikuu vyote, tukawaambia kuwa ni maelekezo ya Rais haya, lazima tuwe na benki ya Ushirika.
Wanaushirika walikubali kutoa sehemu ya mapato yao ya tozo wanazozipata ili kujenga na kununua hisa kwa mara ya kwanza. Mkutano ule ulizaa makusanyo ya zaidi ya bilioni 12. Ninawashukuru sana vyama vikuu vya Ushirika kwa kuwa walielewa dhamira ya Serikali.
Mheshimiwa Rais, naomba nitumie nafasi hii vilevile kukishukuru chama, na niseme tu mbele yako, Mwenyekiti wa CCM wa sasa leo hii tutakukabidhi hati yako wewe kama mshiriki wa benki hii, ulinunua hisa wewe binafsi. Lakini pia ndugu yangu Chongolo, akiwa katibu Mkuu wa CCM, tulimfuata akanunue hisa. Nikamwambia anunue hisa ili kujenga uhalali wa hili jambo, Alikubali kununua na sasa naye ni mshiriki.
Ntoa shukani pia kwa Katibu Mkuu mstaafu Dkt. Bashiru ambaye naye alinunua hisa akiwa kama backbencher ndani ya Bunge. Nakushukuru sana kwa hilo.

Mheshimiwa Rais, leo tunatimiza miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita, na vizuri ikaingia kwenye kumbukumbu kuwa binadamu tumepewa sifa ya usahaulifu. Binadamu husahau. Hata leo tunapozindua benki hatuwezi kukumbuka kuwa miaka 40 wakulima walikuwa hawana benki. Baada ya wiki tutasahau. Lakini maandiko yametukumbusha tukumbushane.
Mheshimiwa Rais, nataka hadhira hii ielewe kuwa ulihutubia Bunge mwaka 2021. Nchi hii haikuwa na “subsidy scheme”. “Subsidy scheme” ya mwisho ilitekelezwa na Serikali ya Awamu ya Nne, na baada ya hapo mwaka 2017, ndani ya Bunge, Bunge likapitisha sheria ya kufuta mfuko pekee uliokuwepo wa kuwasaidia wakulima Export Levy.

Ulivyorudi wewe mwaka 2021, leo na mimi nikiwa na ujasiri, na niko tayari mtu yeyote anichallenge nathubutu kusema kuwa hii ndiyo Serikali inayofanya “the largest subsidy scheme” kwenye nchi zote kusini mwa Afrika.
Mheshimiwa Rais, kwa mwaka 2024/2025 Serikali unayoiongoza inatumia bilioni 99.5 kwa ajili ya ruzuku ya zao la pamba. Mheshimiwa Rais, kwenye zao la tumbaku, Serikali unayoiongoza inatumia jumla ya bilioni 21 kwa ajili ya ruzuku ya tumbaku.
Mheshimiwa Rais, kwenye zao la korosho ambalo watu wote mwaka huu tumeshangilia, na tumekuwa na uzalishaji ambao toka tupate uhuru hatujawahi kuufikia wa tani 520,000 na kitu, wewe mwenyewe umetoa jumla ya bilioni 281 kama pembejeo za miche, na wakulima wanapewa bure. Wakulima kwenye msimu huu uliopita, Mheshimiwa Rais, wameuza mazao yenye thamani ya trilioni 1.5. Ni fedha za wakulima mfukoni. Na mwaka huu tunatarajia “export value” ya zao la korosho itaongezeka kufikia shilingi trilioni 1.8–1.9 kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Rais, huu ni mwaka wako wa tatu unatekeleza ruzuku ya mbolea. Wakati unazungumza na Bunge, matumizi ya mbolea ya nchi hii yalikuwa tani 330,000. Msimu uliopita wa kilimo wa 2023/2024 tumetumia jumla ya tani 860,000. Na msimu huu tunatarajia matumizi ya tani 1.2 milioni. Kwa jumla mpaka sasa umetoa jumla ya bilioni 653 kama ruzuku ya kwenye mbolea.

Mheshimiwa Rais, Serikali yako mwezi wa nane mwaka huu imezindua programu ya “mechanization” pale viwanja vya Nane Nane, na nchi hii, kwenye kusini mwa Jangwa la Sahara, mpaka kufikia mwaka 2025/2026, 2026/2027, 2027/2028, nchi hii itakuwa na “Mechanization Centres” 1,000. Jumla ya matrekta 10,000 yananunuliwa na Serikali, pamoja na “power tillers”, “combine harvesters”. Na Mheshimiwa Rais, sasa hivi tunavyoongea tumeshanunua vifaa vya kuchimbia visima kwa ajili ya wakulima. Tutakuwa na magari mawili makubwa kati ya 20 tunayonunua ya kuchimbia visima. Magari hayo mawili yatakuwa na uwezo wa kuchimba visima vya hadi mita 1,500 kwenda chini kwa ajili ya kuyatafuta maji.
Mheshimiwa Rais, programu hii ya “mechanization” Serikali unayoiongoza itatumia trilioni 1.2 kwa ajili ya “mechanization centres”. Tumefanya “pilot” kwenye pamba, ambapo wakulima wa pamba waliokuwa wanakodi trekta kwa wastani wa Tsh 70,000 hadi 100,000 wamelimiwa mwaka huu kwa Tsh 35,000 kwa ekari. Itakuwa ni “mechanization centre” ambayo ni “service centre” kwa ajili ya kutoa ruzuku kwa wakulima.
Mheshimiwa Rais, umetoa ruzuku ya mbegu kwa mara ya kwanza ndani ya Serikali unayoiongoza. Umetoa ruzuku kwenye mbegu ya mahindi, alizeti, ngano. Mbali na hapo, Mheshimiwa Rais, sekta hii ya kilimo mwaka 2021 mikopo yote iliyokuwa inaenda moja kwa moja kwa wakulima ilikuwa ni bilioni 800. Leo, mikopo iliyoenda kwenye sekta ya kilimo ni trilioni 4, bilioni 270.
Mheshimiwa Rais, kwa mara ya kwanza toka nchi hii ipate uhuru, umetoa ruzuku ya uzalishaji lakini pia umetoa ruzuku katika bei ya wakulima. Kwa mara ya kwanza National Food Reserve Agency uliipa kibali na hivi karibuni tunazindua “Food Security Bond”. Namshukuru Waziri wa Mipango ameshaidhinisha. Naishukuru pia Wizara ya Fedha wameshaidhinisha.

Hifadhi ya chakula ya nchi yetu umeifikisha tani 700,000 ambayo hatujawahi kufika toka tunapata uhuru. Lakini pia Mhe Rais ulikubali bei za mahindi zilivyoanguka zikawa Tsh 300, 400. Ukaniagiza tununue kwa bei ya chini ya Tsh 700 kwa wakulima. Umewapa mbegu, umewapa mbolea, wakakosa soko Serikali ikaingilia kwa ajili ya kuwabeba na inahifadhi mazao. Na niwahakikishie wakulima kwamba safari hii tumejiandaa vilevile kwenda sokoni kwa ajili ya kununua mazao ya wakulima.
Mheshimiwa Rais, nini maana ya hatua hizi zote ulizochukua? Mheshimiwa Rais, leo wakati unahutubia Bunge, ukuaji wa sekta ya kilimo ulikuwa asilimia 2.7. Mwaka 2023/2024, ukuaji wa kilimo umefika asilimia 4.2. Mwaka huu tunatarajia kufika asilimia 5, Huku tukitambua kuwa Malengo uliyotupa ni kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.
Mheshimiwa Rais, wakati unaingia madarakani, “average export value” ya nchi yetu ilikuwa ni dola bilioni 1.2 kwa wastani. Leo, 2023/2024, wastani wa mauzo ya mazao ya nje ya sekta ya kilimo ni dola bilioni 3.5.
Usalama wa chakula umefika asilimia 120. Leo Tanzania kwa ujasiri tunaweza kusema sisi ni wazalishaji wa pili wa mahindi Afrika, wazalishaji wa pili wa zao la tumbaku. Kwa sababu kwenye zao la tumbaku, sisi tulikuwa hatupo kwenye namba moja hadi tano tulikuwa kwenye kundi linaloitwa “wengineo”, ndio tulikuwa huko. Ndani ya miaka mitatu, leo Tanzania ni mzalishaji wa pili wa tumbaku Afrika.
Mheshimiwa Rais, leo Tanzania baada ya Brazil ndio nchi yenye “single own processing plant” ya tumbaku iko Morogoro. Kiwanda cha pili kwa ukubwa kipo Tanzania baada ya Brazil.

Mheshimiwa Rais, ulizindua mpango wa BBT na kulikuwa na mjadala mkubwa sana kwenye nchi yetu, kama ulivyokuwa mjadala wa Benki ya Ushirika. Mnaanzisha Benki ya Ushirika kwa nini? Ningependa kuchukua nafasi hii kuwaambia wenzetu TADB, kisera, ni benki ya maendeleo (Development Bank). Bahati mbaya bungeni ilikuwa: “Kwanini TADB haipo Nzega? Kwanini haipo Igunga? Kwanini haipo Njombe?” Haiwezekani TADB kwenda kuwa katika miundombinu ya biashara (commercial). Ni benki ya maendeleo ambayo inatakiwa iwekeze kwa muda mrefu, itoe “guarantee scheme” kwenye benki za biashara.
Tulianzisha Benki ya Coop kama benki ya kibiashara (commercial bank), ya wakulima, na inayomilikiwa na wakulima, ambayo itafanya kazi za kibiashara. Baada ya kukosekana kwa benki ya wakulima inayofanya kazi za kibiashara, TADB ilibidi ichukue nafasi ile kutoa mikopo kwa wakulima wadogo kama wanavyotoa NMB na CRDB.
Ujio wa benki hii, Mheshimiwa Rais, utairudisha TADB kwenye mamlaka yake ya awali ili iweze kutoa mikopo ya muda mrefu na nafuu kwa ajili ya “infrastructure development” kwenye sekta ya kilimo. Na Benki ya Ushirika ifanye kazi ya kutoa mikopo ya muda mfupi kwa wakulima na mikopo ya pembejeo, ili tuweze kupunguza hatari (de-risk) katika sekta hii ambayo imekuwa kwenye hatari kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Rais, Benki hii uliyozindua leo tunakushukuru sana kwa kukubali Serikali kuwekeza asilimia 10, lakini vilevile ukatoa shilingi bilioni 5 ili washirika waweze kumiliki asilimia 51. Tunakushukuru sana.
Ombi langu, Mheshimiwa Rais, ambalo naliomba kwa dhati: unatoa fedha za pembejeo, unatoa fedha kwa ajili ya “mechanization”, ruzuku, umwagiliaji. Na Serikali unayoiongoza naishukuru sana na uzuri Mheshimiwa Aweso yupo hapa kwa sababu uwekezaji wa sekta ya umwagiliaji kama hakuna “alignment” na mwenye maji ni mtihani. Nashukuru Aweso kwa kuwa “flexible”. Wamekuwa tayari kuturuhusu tudizaini miradi ya umwagiliaji kwenye mabonde. Tunatekeleza miradi 780 katika nchi yetu yenye jumla ya hekta 560,000, ambayo kila mwaka unawekeza karibu bilioni 300.

Serikali unayoiongoza imeanza kujenga mabwawa zaidi ya 114 katika nchi yetu kwa ajili ya kuvuna maji. Umetupa maelekezo, na Mheshimiwa Aweso tutangaze mradi wa kujenga kutoka Ziwa Victoria kuleta Dodoma, kama gridi ya taifa ya maji, ili ihudumie binadamu, wanyama, na mifugo.
Uwekezaji wote huu, Mheshimiwa Rais, kama Benki Kuu yetu haitokubali kufanya mageuzi kwenye modeli ya kifedha ya nchi yetu, na sisi kama nchi kuwa na sera ya kwanza ya “Agricultural Financing Policy” ambayo italeta mfumo wa ukopeshaji kwenye sekta za uzalishaji kwa maana ya kilimo, mifugo na uvuvi tofauti na mifumo ya sasa ya kifedha, bado tutakuwa na safari ndefu ya kumwondoa mwananchi huyu maskini katika umaskini uliopo.
Kwa sababu watahitaji kuwa na mifumo sahihi, “incentive scheme” ambazo benki za biashara zitapewa ili ziweze kumkopesha mkulima tofauti na wanavyomkopesha muuza duka, Bakhresa, au mwingine yoyote.
Mkulima na sekta ya kilimo wanahitaji unafuu tofauti kabisa na bidhaa zilizopo sokoni pamoja na hatua zilizoko sokoni. Mheshimiwa Rais, ili tusiivuruge Benki ya Ushirika (CoopBank), umenipa maelekezo kuwa kutakuwa na dirisha maalum ndani ya benki ya Ushirika. Dirisha hili litakuwa maalumu kwa ajili ya AGITIF, na Mheshimiwa Rais umetusaidia kuomba fedha za BBT kutoka ADP. Watu wengi wamekuwa wakihoji kuhusu maendeleo ya BBT. Tumepata dola milioni 29 ambazo zitatekeleza mradi wa BBT kupitia Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Programu hii, Mheshimiwa Rais, wakati tunasaini mradi huu, tuliomba kuwepo kwa dirisha la fedha la dola milioni 35. Fedha hizi, Mheshimiwa Rais, zitakusanywa kupitia sekta ya kilimo na kisha zitaelekezwa kama dirisha maalumu ndani ya Benki ya Ushirika, ambapo zitafanya kazi ya kutoa mikopo kupitia mpango wa dhamana (guarantee scheme) na pia zitumike kama mfuko wa mtaji wa usawa (equity fund) kwa wenye miradi ya kilimo. Lengo ni kuhakikisha riba iwe nafuu, tofauti na mikopo ya kibiashara ambayo benki ya Ushirika itaendelea kutoa kwa huduma nyingine.
Lakini mbali na hapo, kama Wizara tunaendelea kutenga fedha za AGITIF katika bajeti ili kuiwezesha AGITIF kuwa na mitaji nafuu. Fedha hizi zitaelekezwa kwenye dirisha la CoopBank, na Coop atafanya kazi ya kuwakopesha wakulima kwa riba nafuu. Kwa sasa, wanachukua mkopo kwa riba ya asilimia 7, lakini wakipelekewa wakulima inakuwa asilimia 11 hadi 15, jambo ambalo litakuwa halijafikia lengo letu. Kwa hiyo, fedha hizi zitakazotengwa kwenye mfuko wa AGITIF, mara kwa mara, zitasimamiwa kupitia CoopBank na zitakuwa sehemu ya dhamana na mtaji wa usawa (equity fund), kwa ajili ya kupunguza hatari (de-risking) kwa wakulima na kuwapatia mitaji ya mikopo yenye riba ya tarakimu moja. Hazitatoka serikalini zikiwa na riba inayozidi asilimia 2 hadi 3.

Mheshimiwa Rais, sisi kama wakulima tumeibeba sekta ya uchumi wa nchi hii kupitia kilimo. Natumia fursa hii kwa niaba ya wakulima kukushukuru sana kwa dhati kwa kuliona jambo hili na kuona kuwa wakulima ni watu wanaostahili kupewa mkono ili waweze kupambana katika huu uchumi wa kibepari.