Tarehe 21/9/2025 Nzega Mjini imefurika  maelfu ya wananchi waliokusanyika kumsikiliza mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Hussein Bashe, katika mkutano mkubwa wa kampeni uliojaa shamrashamra na hamasa kutoka makundi mbali mbali. 

Akiwahutubia wananchi wa Nzega Mjini Mhe, Bashe amezungumza kwa kina kuhusiana historia yake ya kisiasa, mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chake cha uongozi na dira ya maendeleo kwa miaka mitano ijayo.

Bashe amebainisha kuwa historia yake imekuwa na mapito mengi, lakini amahidi kuendelea kuwalinda na kuwatunza wana CCM na wananchi wote waliolilea na kulitunza jimbo hilo,

Mimi si mtoto wa magorofani. Nimezaliwa hapa Nzega, uswahilini. Tunafahamiana na tunajua shida zetu. Historia yangu mnaijua, nilipotoka shule mwaka 2005 nilikuja kuomba kura hapa. Wakati huo masela walinichapishia mabango ya black and white, wakasimama nami mpaka nikachaguliwa. Mwaka 2010 nilirudi tena, nikapata kura 14,000, mpinzani wangu alipata kura 2,000, lakini chama hakikuniteua. Nilirudi nikawaambia wananchi mchagueni chama. Tukaendelea na safari ya maendeleo.”

Akikumbushia  tukio la mwaka 2015, Hussein Bashe amesema kuwa anakumbuka katika serikali ya awamu ya tano alimwambia hayati Dkt. John Pombe Magufuli alipokuja Nzega kuwa kwamba hataki chochote bali mambo mawili muhimu kwa wananchi wa Nzega: huduma ya maji na kurejesha eneo la wamachinga. Amebainisha kuwa, kwa wakati huo migodi ilikuwa imekwisha, na shughuli zilizobaki zilikuwa ni biashara ndogondogo za wamachinga. “Nilisimama nikasema eneo hili libaki kuwa la wamachinga. Na kweli tukaachiwa eneo hilo.”

Bashe pia amebainisha namna alivyomweleza Rais Samia Suluhu Hassan alipotembelea Kata ya Mbogwe kuhusiana na changamoto kubwa ya Maji Nzega Mjini.

“Nilimwambia mama sina jingine zaidi ya maji. Leo ninamshukuru Rais Samia, kwa sababu ndani ya miaka minne, kata zote kumi, vijiji vyote 21 na vitongoji vyote 176 vya Nzega vina maji. Tumepiga hatua kubwa, na sasa tunaanza hatua ya pili kuhakikisha tunaondokana na utegemezi wa Kashwasa.”

Bashe ameeleza pia kuwa katika miaka mitano ijayo  tutegemee ujenzi wa chujio jipya katika bwawa la Kilimi ukianza kama  mbadala wa maji ya Ziwa Victoria, mradi ambao tayari umeidhinishwa na Serikali.

Bashe ameendelea mbele na  kuwambia wana Nzega kuwa kwa sasa ndiyo jimbo pekee kati ya maeneo yanayopokea maji kutoka Ziwa Victoria ambalo hulipa shilingi 1,500 kwa unit ya maji, wakati maeneo mengine hulipa kati ya shilingi 2,000 hadi 2,200. Akifafanua kuwa siri ya unafuu huo ni hatua aliyochukua binafsi mwaka 2010 kumshawishi aliyekuwa Naibu Waziri Kamwele kuunganisha bwawa la Kilimi na mtambo wa maji wa Ziwa Victoria.

Nusu ya maji tunayoyatumia leo yanatoka Kilimi, nusu yanatoka Victoria, ndiyo maana tunalipa 1,500,” ameeleza Mgombea

Mgombea ubunge pia ameeleza hatua kubwa zilizopigwa katika sekta ya elimu na afya jimboni hapo. Ambapo mwaka alipochaguliwa kwa mara ya kwanza wanafunzi waliokuwa wakiendelea na masomo ya sekondari walikuwa wachache mno takribani 47, lakini sasa zaidi ya wanafunzi 650 wamejiunga na vyuo vya kati, huku sekta ya elimu ikiendelea kupewa kipaumbele kwa kujengwa shule mpya, mabweni na shule ya wasichana Mwazogi kuanza kupanuliwa kufikia kidato cha tano na sita. Na Katika afya, kata zote sasa zina zahanati, vituo vipya vya afya vimeanza kujengwa na tayari ujenzi wa hospitali ya rufaa umeanzishwa.

Katika upande wa biashara na uchumi, Bashe amewaeleza wananchi kuwa fedha zimepatikana kwa ajili ya kujenga soko kuu la machinga na parking kubwa ya kisasa kwa ajili ya wafanyabiashara. Akiwahakikishia wananchi kuwa hakuna mtu atakaye nyang’anywa kibanda chake, bali kila mwenye kibanda atasajiliwa rasmi na baada ya ukarabati wa masoko na maeneo ya wamachinga atarejeshwa sehemu yake ya awali. 

Amebainisha pia kuwa tayari tenda imetangazwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami kilomita kumi kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, na masoko mapya ya Kachoma na Machinjioni yamepata wakandarasi.

“Tutajenga soko la nafaka, soko la ushirika, na eneo la Kikwete tutaligeuza kuwa sehemu ya watoto kucheza, kwa sababu mji wetu unakua na tunataka vijana na watoto wetu waishi kwenye mazingira bora zaidi,” alisema Bashe.

Vilevile, ametaja miradi ya kimkakati ya kitaifa inayotekelezwa Nzega ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Chuo cha VETA, shule ya amali, kituo kikubwa cha kuhifadhi nafaka katika eneo la Njiro, hospitali ya shufaa na rufaa, pamoja na stendi na parking mpya za malori zitakazoboresha biashara na usafirishaji.

Akihitimisha hotuba yake, Bashe amewashukuru wananchi wa Nzega kwa mshikamano waliouonesha kwa miaka yote ya uongozi wake, akisisitiza kuwa safari ya maendeleo bado inaendelea.