Dodoma, Machi 2025
Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb), ameipa Bodi ya Chai Tanzania (TTB) muda wa siku 14 kuwasilisha taarifa kamili ya gharama za uzalishaji na uchakataji wa chai nchini, kwa lengo la kuweka msingi wa maboresho ya bei na tija katika tasnia hiyo muhimu kwa uchumi wa wakulima na nchi kwa ujumla.

Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Wadau wa Chai uliofanyika jijini Dodoma, Waziri Bashe amesema kuwa ni muhimu kufahamu gharama halisi kutoka ngazi ya mkulima hadi kiwandani, ili kuweka mifumo ya usimamizi na bei inayomlinda mkulima na kuvutia uwekezaji.
“Nataka ndani ya siku 14 niwe nimepata taarifa rasmi ya gharama hizi. Bodi ya Chai ikae na wadau wake, watengeneze timu ya kiufundi na walete taarifa hiyo,” amesisitiza Waziri Bashe.
Aidha, Mhe. Bashe ametangaza mikakati ya kuongeza thamani ya chai ya Tanzania kwa kusisitiza uuzaji wa chai iliyochakatwa badala ya majani ghafi. Tayari Bodi imenunua mashine tatu za kuchakata na kuchanganya chai, ambapo mashine hizo zitafungwa katika maeneo ya Korogwe (Dindira) na ghala la Kipawa jijini Dar es Salaam, na kukabidhiwa kwa AMCOS kwa makubaliano maalum.
Waziri Bashe pia amezindua rasmi chapa ya taifa ya chai ya Tanzania na kuhimiza wachakataji, wachanganyaji na wafungashaji kuitumia chapa hiyo kwenye vifungashio vyao ili kuimarisha utambulisho wa chai ya Tanzania kimataifa.

“Chai yetu inapaswa kujulikana kuwa ni ya Tanzania. Hatuwezi kuendelea kuuza bidhaa yetu kwa jina la nchi nyingine. Kupitia chapa ya taifa, tutaimarisha soko letu ndani na nje ya nchi,” alisema.
Kupitia jitihada za serikali na Bodi ya Chai, masoko mapya ya kimataifa yamefunguliwa katika nchi za Oman, Qatar, UAE, Japan na Saudi Arabia. Kampuni ya Mponde Holdings tayari imesaini mkataba wa kuuza tani 100 za chai kila mwezi nchini Oman, huku mazungumzo yakiendelea kwa mkataba wa tani 260 kwa mwezi na wanunuzi kutoka Urusi na Dubai. Kampuni ya Kazi Yetu nayo imesaini mkataba wa kuuza chai maalum nchini Qatar.
Mhe. Bashe amesema hadi kufikia Machi 25, 2025, mauzo ya chai nje ya nchi yamechangia Shilingi bilioni 50.25 kwa taifa, huku serikali ikiendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kupitia bajeti ya mwaka 2024/2025 ikiwemo Mradi wa Ustahimilivu wa Usalama wa Chakula katika mikoa ya Kilolo, Njombe na Mbeya.

Ametaja baadhi ya wawekezaji wapya akiwemo Kampuni ya ITO EN ya Japan inayonunua majani kutoka shamba la NOSC na Kampuni ya Hong Ding Xin Investment Ltd inayojenga kiwanda cha kuchakata chai maalum Kilolo.
Waziri Bashe pia amegusia changamoto zinazoikumba sekta ya chai ikiwemo kushuka kwa bei kimataifa, uhaba wa dola kwenye baadhi ya masoko, na athari za vita katika maeneo mbalimbali duniani. Hata hivyo, amesema serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuondoa tozo ya VAT na AMT hadi Juni 2027 kwa viwanda vya kuchanganya chai, na kuwapatia wakulima wadogo mashine za kuchakata.

Mnada wa chai wa Dar es Salaam unaofanyika kila Jumatatu pia umeendelea kuimarishwa kwa kuongeza madalali na kuboresha miundombinu ya mnada huo katika ghala la Kipawa.
Waziri Bashe amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wakulima, wawekezaji na wadau wote ili kuhakikisha chai ya Tanzania inachangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa viwanda, ajira na kipato cha wananchi.