


Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb), amekutana kwa mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa Uingereza kwenye Sekta ya Biashara, Mhe. Lord Walney na kujadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano kafika Sekta ya Kilimo.
Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na maendeleo ya utafiti wa kilimo, hifadhi ya mazingira, lishe, miundombinu na rasilimali fedha kwa ajili ya kumkwamua mkulima.
Waziri Bashe amehamasisha Serikali ya Uingereza kuelekeza rasilimali kwenye miradi itakayowawezesha wakulima moja kwa moja kiuchumi; ambapo alitoa mfano wa uwekezaji kwenye miundombinu ya umwagiliaji kama njia mojawapo ya kumsadia mkulima asiharibu mazingira kwani atakuwa na uhakika wa kulima na kuvuna katika vipindi vyote vya mwaka bila kutegemea mvua.
Aidha, Waziri Bashe amefafanua zaidi kuwa katika misimu ya kiangazi wakulima wasio na miundombinu ya umwagiliaji hugeuza shughuli zinazoharibu mazingira, ikiwemo uchomaji wa mkaa kama mbadala wa kujipatia kipato.
Mhe. Lord Walney aliambatana pia na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. David Concar na Mshauri wa Ubalozi huo katika masuala ya Teknolojia ya Kilimo na Uchumi wa Buluu, Bw. Godfrey Lwakatare.